Mashabiki wa Timu ya Zanzibar, Zanziabar Heroes, wakiilaki Timu yao.
Kikosi Cha Timu ya Zanzibar, Zanzibar Heroes
Nahodha wa timu ya Zanzibar Hereos Nadir Haroub Kanavaro
akiishukuru Serekali ya Zanzibar kwa mashirikiano iliyotoa kwa timu hiyo.
Naibu Waziri wa Habari,Utamadu Utamaduni na Michezo Bi Hindi
Hamadi akiwashukuru wa wachezaji pamoja na viongozi wao kwa ushindi walio upata
wa nafasi ya tatu katika mashindano ya Challenge Uganda.
************************
NA HABARI MAELEZO, ZANZIBAR
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema imefurahishwa sana
na kiwango cha mchezo kilichooneshwa na Timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar
Heroes) katika Mashindano ya Challenge licha ya kuambulia mshindi wa tatu wa
mashindano hayo.
Aidha katika kuipongeza Timu hiyo Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein amepanga kukutana na
Vijana hao ikiwa ni pamoja na kubadilishana mawazo ya kuimarisha kikosi cha
Timu hiyo.
Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Utalii na Michezo Bihindi
Hamad Khamis ameyasema hayo ukumbi wa Hoteli ya Bwawani wakati alipokuwa
akizungumza na Timu hiyo mara baada ya kuwasili Zanzibar kutoka Uganda.
"Naleta salamu Rasmi za Serikali kwa juhudi kubwa
mliyoifanya kule Uganda na Rais kasema atapanga siku ya kukutana nanyinyi ili
mbadilishane naye mawazo ya kuboresha timu zaidi" alisema Bihidi.
Amesema juhudi ambazo zilioneshwa na Vijana wa Zanzibar
Heroes zinafaa kuthaminiwa kutokana na kucheza na timu ziliozojaa uzoefu na
wachezaji maarufu lakini vijana hao walipigana kiume na kuambulia nafasi ya
tatu.
Bihindi amewataka Wachezaji wa Zanzibar Heroes kutunza afya
na kuimarisha mazoezi yao ili michuano ya mwakani waweze kuwaletea Wazanzibar
kikombe cha Ushindi wa Mashindano hayo.
Ameongeza kuwa kiwango cha mchezo walichoonesha vijana hao
kiliwasisimua Wazanzibari wengi na kuwasababisha kutenga muda wao kwa ajili ya
kuangalia timu yao kila ilipokuwa ikicheza.
Aidha aliwataka Wachezaji hao kuitumia fursa ya kuonana na
Rais kuelezea mipango wanayodhani itakuwa bora katika kuimarisha Timu hiyo kwa
faida yao na Taifa kwa ujumla.
Kwa upende wake Meneja wa Timu ya Zanibar Heroes Salim
Msabah ameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kushirikiana bega kwa bega na
Chama cha Soka Zanzibar ZFA katika kuhakikisha timu inapatiwa maandalizi ya
mapema ndani na nje ya Nchi ili kuimarisha kikosi cha timu hiyo.
Amesema anaamini Zanzibar kuna vipaji vya kutosha katika
fani ya Soka na hivyo kinachohitajika ni namna bora ya kuviendeleza vipaji hiyo
ikiwa ni pamoja na maandalizi ya mapema.
Nahodha wa Timu hiyo Nadir Haroub amesema lengo lao lilikuwa
kutwaa Ubingwa wa Michuano hiyo lakini nafasi waliyoipata ya Mshindi wa tatu
imewafariji kutokana na kuifunga timu pinzani kwao.
Amedai kuwa ushindi huo pia utawajengea heshima wale
wachezaji wa Zanzibar wanaocheza Soka katika ligi ya Bara kutokana na kuifunga
Kilimanjaro Stars ambayo wanacheza wake wanacheza wote katika ligi hiyo.
Timu ya Zanzibar Heroes iliibuka Mshindi wa Tatu wa
Mashindano ya Challenge yaliyofanyika nchini Uganda baada ya kuichapa
Kilimanjaro Stars kwa mikwaju ya Penalti 6-5 na kufanikiwa kupata zawadi ya
kitita cha Dola za Marekani 10,000.